TAFUTA

Friday, August 17, 2012

SIASA NA UCHUMI

DEMOKRASIA SIASA NA UCHUMI, DEMOKRASIA
Na mwandishi wetu
17th August 2012
KWA Tanzania, kama ilivyokuwa kwa nchi nyingine za dunia ya tatu, mlango wa karne ya 21 ulifunguka kwa kishindo, huku wapangaji wawili wakishindana mbio kuingia kuiteka sebule kwa mbwembwe ikiwa ni ishara ya ukuu kwa mshindi miongoni mwa wapangaji.
Washindani hawa wa mwanzo ni mabwana “Uhuru wa Kisiasa”, kwa jina jingine “Demokrasia ya Siasa”, na “Uhuru wa Kiuchumi” au “Demokrasia ya Kiuchumi”, kwa jina la pili.
Injili ya kila mmoja ni kwamba taifa haliwezi kuifikia “mbingu” ya maendeleo ila kwa njia ya yeye. Tuliisikiliza injili hiyo, kila mmoja kwa tafsiri yake huku wakigongana vichwa na kupigana vikumbo wao kwa wao hadi waasisi wa injili hiyo walipotuambia kwamba kwa injili zote mbili ni safi, zinakwenda sambamba ili kutuwezesha hima kuiona mbingu ya maendeleo.
Ndipo tukaanza kufafanuliwa kwamba uhuru wa kisiasa (political liberty) maana yake ni kugawa madaraka ya kisiasa kwa wengi. Tukaelezwa kwamba madaraka yote hulevya, lakini madaraka makubwa hulevya zaidi; na kwamba uhuru wa kisiasa hauji inapokuwa kwamba madaraka ya nchi yameatamiwa na kikundi kidogo cha watu wachache wanaoamua kila kitu kuhusu mwelekeo wa nchi.
Tukatikisa vichwa kama ishara ya kukubali wafanyavyo wazee wenye busara; mbingu zikafunguka na mwanga ukaangaza kuashiria mfumo wa vyama vingi vya siasa. Lakini, hata hivyo, ilikuwa anga tupu, hatukuweza kuyaona maendeleo.
Kisha tukasikiliza tafsiri na maana ya “Uhuru wa Kiuchumi”, kwamba kama ilivyo kwa uhuru wa kisiasa, uhuru wa kiuchumi, (economic liberty) ni kitendo cha kumilikisha uchumi wa nchi kwa wengi badala ya uchumi huo kumilikiwa na wananchi kupitia mkono wa serikali. Kwa maana nyingine, serikali haipashwi kujiingiza katika suala la kupanga na kuongoza uchumi.
Hapo tena mbingu zikafunguka na mwanga ukaangaza; tukaanzisha soko huria, ubinafsishaji wa njia kuu za uchumi kwa kasi ya kutisha, tukafungua milango kwa umilikaji wa rasilimali za taifa kwa wageni, madini na ardhi.
Lakini hata hivyo, maendeleo yakatupiga chenga, tukabaki kuduwaa. Tukaambiwa kesheni taa zenu ziwake daima; maana hamjui saa ya kuja kwa bwana maendeleo; mchana au usiku.
Tukaambiwa tena; “maendeleo hayaji kwa injili ya mazingira ya nchi pekee hasa ikizingatiwa kwamba injili ya ufalme wa siasa na uchumi sasa imehubiriwa ulimwenguni kote, wengi wakaijua, wakisikia ikihubiriwa. Tukaaswa, kuyasaka maendeleo.
Tukaelezwa, ili tuendelee lazima tushikamane na wale ambao tayari walikwisha endelea, na katika kufanya hivyo lazima tufuate njia waliyopita “wenzetu” walioendelea. Muungano huo wa “kimaendeleo” unaitwa “utandawazi”, na ndiyo injili kuu ambayo inahubiri kwamba yote yatakuwa mapya: shida na chuki zitatoweka kwa wote; “mwana kondoo na simba watachanganyika bila hofu, na mtoto mdogo atachezea tundu la nyoka” salama.
Kama usemi wa wahenga kwamba, “huwezi ukatumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja” ni wa kweli, je, inawezekana uhuru wa kisiasa na uhuru wa kiuchumi kwenda pamoja wakati mmoja kwa mafanikio? Kama sivyo, kipi kianze?
Maoni ni kwamba vyote viwili ni muhimu kwa maendeleo lakini haviendi pamoja wakati mmoja. Ni sawa na uhusiano wa yai na kuku. Hivi kati ya yai na kuku kipi kilitangulia?
Tunaambiwa tufuate njia za nchi zilizoendelea; je, ni kweli zilipita njia tunayopita hivi sasa? Ni ipi iliyo sahihi kwa maendeleo, kati ya injili ya kuimarisha kwanza uchumi wa ndani au Utandawazi?
Kwa hali ilivyo hapa kwetu, nini kitangulie kati ya hivyo viwili? Je, ni sahihi kufanya tunavyofanya, kwa manufaa ya maendeleo?
Ni ukweli usiopingika kwamba, wakati uhuru wa kiuchumi umepiga mbio kwa kasi maradufu, kama inavyojidhihirisha kwa ubinafsishaji na umilikishaji wa uchumi wa taifa kwa wageni badala ya kuwamilikisha wananchi (chunga ulimi wako, usiseme “wazawa”), uhuru wa kisiasa unachechemea huku umefungwa minyororo kwa makusudi.
Kwa mfano, Katiba ya nchi ya mwaka 1977 iliyodumaa; mbali na mabadiliko kidogo yaliyoruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa, sehemu kubwa ya Katiba hiyo inabakia kama ilivyokuwa na kwa matarajio ya utawala wa Chama kimoja, miaka 35 iliyopita.
Chaguzi zote si huru na za haki; rushwa na “takrima” imetawala kiasi kwamba fedha inanunua madaraka na madaraka nayo yananunua utajiri. Chaguzi zinapotawaliwa na rushwa, uhuru wa kisiasa hufa na demokrasia hugeuka kejeli kwa umma.
Wakati uhuru wa kiuchumi unaruhusu mtu atambe apendavyo kadri “akili” yake inavyomruhusu, kwa mfumo wetu wa siasa, mtu huyo huyo haruhusiwi kugombea nafasi ya uongozi ila kwa kupitia chama cha siasa tu. Na kwa kuwa “vigogo” wanaopata madaraka kwa nguvu ya fedha na utajiri, wanajuana kwa “mizengwe” kama Waarabu wa Pemba wajuanavyo kwa vilemba vyao, mtu wa kawaida hapati nafasi wala uhuru wa kuwania madaraka na uongozi.
Hii ndiyo sababu hoja ya “mgombea binafsi” inapigwa nyundo kila mara inapojaribu kuinua kichwa. Na hata kama masikini huyo atagombea kwa tiketi ya chama na atapokonywa ushindi halali kwa nguvu ya fedha, hawezi kuitetea haki yake kwa sababu hatakuwa na shilingi milioni tano za kufungulia kesi ya kupinga kupokonywa haki hiyo.
Sababu hizi zikufanya uamini kwamba nchini kwetu uhuru wa kisiasa umepigwa nyundo na kutoa kipaumbele kwa uhuru wa kiuchumi kwa manufaa ya “walio nacho” dhidi ya “wasio nacho”. Hakika katika mazingira ya aina hii, hatuwezi kupata maendeleo ya kweli kwa raia wote.
Uhuru wa kisiasa unawawezesha watu kushiriki katika ngazi zote za jamii yao, na kwa kufanya hivyo jamii nzima inanufaika na mchango wao wa mawazo.
Utawala wa kidemokrasia hauwezi kuwa safi siku zote, hata iweje. Kwa hiyo, ni kwa njia ya kuishirikisha jamii pana zaidi kwa pande kinzani katika jamii zinaweza kufikia mwafaka kwa maendeleo ya nchi. Vijembe na kejeli kama vile “wapeni vidonge vyao, wakitema, wakimeza ni shauri yao”, ni ukiritimba wa mawazo usiojenga, ni uhasama adui kwa demokrasia unaokaribia “unyang’au”.
Je, ni kweli kwamba uhuru wa kisiasa unachangia kukua kwa uchumi wa taifa? Kuna kambi mbili kinzani zinazojitokeza kuhusu jibu la swali hili. Kambi ya kwanza ni ile inayodai kwamba uhuru wa kisiasa ni sharti moja kubwa katika maendeleo ya kiuchumi; kwamba taifa huru lenye watu huru kisiasa, lina nafasi nzuri ya kupanga na kuongoza uchumi wake bila ya kuingiliwa kwa manufaa ya watu wake kuliko taifa linalotawaliwa na taifa jingine kisiasa. Kwa hili, ukweli wa usemi kwamba “siasa ni uchumi”, lakini “uchumi si siasa” unajidhihirisha wazi.
Kambi hii inaunga mkono wito wa kauli mbiu ya rais wa kwanza wa Ghana, Kwame Nkrumah, kwamba “Utafuteni kwanza ufalme wa kisiasa, na mengine yote mtazidishiwa” (Seek ye first the political kingdom and the rest shall be added unto you).
Kambi ya pili inadai kwamba uchumi wa nchi unaweza kupangika vizuri na kuendelea vema iwapo hautaingiliwa na siasa na wanasiasa.
Wanadai kwamba serikali lazima ijiondoe kabisa katika kupanga na kuongoza uchumi kwa kuiacha nguvu ya soko itawale; na pia kwamba uhuru wa vikundi (umma) na vyama vya wafanyakazi usiruhusiwe kuhoji mwenendo wa uchumi, soko na uzalishaji; wala kusiwe na kuhoji manufaa ya mwenendo huo kwa umma.
Kwa kambi hii, maendeleo ya “miradi” huchukua nafasi ya kwanza badala ya maendeleo ya “watu”. Mjadala huu bado ni hai na tata. Tunaambiwa tupite njia waliyopita wahenga wetu wa maendeleo ili tushikane mikono ndani ya “ufalme” wa Utandawazi. Ni njia ipi iliyo sahihi kati ya hizi mbili?.
Utata huu unaweza kuondolewa tu kwa kuangalia historia ya baadhi ya nchi zilizopitia njia hiyo ya maendeleo, lakini hata hivyo maandishi ukutani yanaonyesha si ya kutarajia.
Mara nyingi historia ya maendeleo ya nchi za Ulaya Magharibi imechukuliwa kama mfano wa kuigwa na nchi masikini za dunia ya tatu. Ni nini walichofanya wao kujikomboa kutoka ufukara wa kutupwa kama tulivyo, kufikia hali ya kujitosheleza kiuchumi?
Ni kipi kilichoanza, uhuru wa kisiasa au kukua kwa uchumi na maendeleo? Au ni kukua kwa uchumi na maendeleo ndiko kulikowezesha mapinduzi (evolution) ya uhuru wa kisiasa?
Tuchukue mfano wa Uingereza ya karne ya 18, kipindi ambacho kinahusishwa na mapinduzi ya viwanda (industrial revolution) ya nchi hiyo. Katika kipindi hicho na miaka iliyofuatia, nchi hiyo iliibuka na mapinduzi kwa kasi ya kushangaza, mapinduzi yaliyoshuhudia mageuzi ya kijamii, umilikaji ardhi na kufutika kwa vijiji sehemu za mashambani.
Kufikia kwaka 1852, Uingereza ilikuwa “karakana” ya dunia ikiongoza katika viwanda, biashara na katika kumiliki rasilimali kubwa za nchi za joto, ikiwamo Afrika.
Je, maendeleo haya yalipatikanaje? Nao uhusiano kati ya uhuru na maendeleo ulikuwaje? Ni wazi kwamba uhuru ulikuwa kwa tabaka la wenye viwanda pekee, yaani watu matajiri wenye mitaji. Kwa wengine katika jamii uhuru ulibanwa na kudhibitiwa. Kwa mfano, vyama vya wafanyakazi vilidhibitiwa ambapo baadhi ya viongozi wake walitupwa uhamishoni kwenye makoloni; vyama vya kiraia (civil society) vilipigwa marufuku pia.
Mageuzi ya kisiasa yalizimwa na yaliruhusiwa pale tu yalipoonekana kuwa ya manufaa kwa waliokuwa madarakani.
Pamoja na hayo, tofauti na ilivyo hapa kwetu hivi sasa, maendeleo ya kiuchumi yalipatikana kwa kutumia nguvu kazi ya watumwa. Utumwa wa sasa ni huu unaoibuka kwa kuwafanya wazalendo kugeuzwa “watumwa” katika nchi zao, wakizalisha lakini bila kupata maendeleo.
Huko Uingereza uhuru wa kisiasa na demokrasia ulipatikana kwa nguvu na wakati mwingine kwa njia ya umwagaji damu ambapo baadhi ya wanaharakati wa uhuru na demokrasia walinyongwa na wengine kupelekwa uhamishoni kwenye makoloni. Wakati huo Uingereza ilitawala karibu robo ya watu wote duniani kupitia makoloni na kutaka “iabudiwe”.
Kwa hiyo, kwa Uingereza, tunaweza kusema kwamba hapakuwa na uhusiano kati ya uhuru wa kisiasa na maendeleo ya kiuchumi kwa watu wake. Kinyume chake kulifanyika hatua za makusudi za kudhibiti uhuru wa kisiasa ili kuruhusu kukua kwa uchumi. Ukiachilia mbali marekebisho madogo madogo ya hapa na pale juu ya uhusiano huu, mfumo huu ndio ulivyokuwa kwa nchi nyingine za Ulaya Magharibi.
Uzoefu wa nchi zetu unatuambia nini? Ni kwamba tofauti na ilivyokuwa kwa Waingereza nchini mwao, wakati wa ukoloni katika nchi zetu, “maendeleo” ya uchumi yalipangwa na kusimamiwa na wakoloni wenyewe bila ya kuwashirikisha wananchi. Walichoambiwa tu ni nini wazalishe, nini kiuzwe wapi, bila kuambiwa ni kwa manufaa ya nani.
Tulipopata uhuru wa kisiasa (uhuru wa bendera?), cha kusikitisha ni kwamba mtindo wa kutowashirikisha wananchi katika kupanga maendeleo yao, uliendelezwa na kuimarishwa zaidi. Nguvu ilitumika kuwanyamazisha waliohoji maana ya uhuru wa visingizio vya kulinda maendeleo. Wote waliohoji waliitwa wapinga maendeleo na adui wa taifa.
Kwa hali hii, yaliyotokea huko nyuma yasichukuliwe kuhalalisha yanayotokea leo, bali uzoefu huu wa kihistoria utumike kama fundisho kutuwezesha kutabiri ya mbele na kuepuka makosa yanayoweza kuepukika.
Je, historia inajirudia enzi zetu za uhuru? Ndiyo, hali inavyoonyesha huenda historia ikajirudia ingawa si kwa msamiati wa kale. Lakini tujiulize, uhuru wa nani? Na kama uhuru huo unapashwa kudhibitiwa kwa sababu zozote zile: ni kwa kiwango gani? Ni nani mwenye uwezo au uhalali wa kutoa maamuzi hayo?
Ni dhahiri kwamba Uingereza isingefikia maendeleo na kukua kwa uchumi wake ilivyofikia bila ya kudhibiti uhuru. Lakini ikumbukwe kwamba ni unyama wa kibepari uliosababisha mtafaruku wa kijamii na uhuru wa mtu binafsi ukapatikana katika nyanja zake zote za maisha. Kama mfano wa Uingereza ni wa kuigwa, je, ina maana tujenge na kuimarisha kwanza ubepari kupata mtafaruku wa kijamii, ili baadaye tuweze kupata uhuru wa kweli, kisiasa na kiuchumi?
Ni ukweli usiopingika kwamba ni katika nchi zenye viwanda pekee ambako uhuru wa kweli wa kisiasa unashamiri. Ni kwa nini tumeshindwa kujenga jamii kama hizi ambamo uhuru wa kisiasa na uhuru wa kiuchumi vinashabihiana, bila kuiga au kuazima sera na mifumo kutoka nje?
Ni kwa sababu tulirithi serikali “legelege” kutoka kwa wakoloni, tukaongozwa na watawala legelege wasio na ujuzi lakini walafi, wenye uchu wa madaraka, wala rushwa, wasiojiamini na wenye kupuuza dhamana waliyokabidhiwa na umma bila hofu ya kuhojiwa.
Viongozi wa aina hii wapo hadi sasa, wakitaka madaraka makubwa zaidi ili kujinufaisha wao wenyewe na marafiki zao. Kwao uongozi si wito wala kuwajibika, bali ni njia moja ya kujinufaisha wao na ndugu zao huku wakijitapa kuleta “maendeleo”, kila mmoja kwa zamu yake, kwa kuonyesha takwimu, wanataka mkate wao wa kila siku.
Uhuru wa kweli ni ule uliofafanuliwa na mababu zetu, kwamba “sema utasikilizwa; omba utapewa”. Tujiulize, haya yawezekana leo?.
Na kwa watawala, somo bora ni lile la mtawala kuwaacha watu wajione wao ndio wanaotawala na hivyo wataweza kutawalika kwa urahisi.
Kama alivyosema mwanafalsafa wa Kichina Lao Tse, karne kadhaa zilizopita, “kiongozi anakuwa mzuri inapokuwa watu wanafahamu kidogo sana kwamba yupo; si kwa kiongozi huyo kutafuta ukuu na kutiiwa; kushangiliwa na kutukuzwa mara kwa mara. Ukiwaheshimu watu, nao watakuheshmu.”
Lao Tse anaongeza: “Kiongozi mzuri ni yule mwenye maneno machache na kazi ikafanyika, na matakwa yake kutekelezwa. Hapo, watu wataweza kusema, ‘ tuliifanya kazi hiyo sisi wenyewe’. ”
Uongozi siku hizi hauna tofauti na umamluki. Tuwaacheni watu wachague mipango yao ya maendeleo wanayoona inafaa, badala ya kuwauza kwa sera mumiani za kimataifa zinazobadilika kila kukicha. Wao ndio wanaojua mahitaji yao, kipi kianze na kipi kifuate.

No comments:

Post a Comment