Kocha wa Taifa Stars,Jan Poulsen
TIMU
ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' inatarajia kucheza mechi ya
kirafiki ya kimataifa na timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Congo (DRC) 'The Leopards' Februari 23 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar
es Salaam.
DRC ndiyo imeomba kucheza mechi
hiyo ya kirafiki dhidi ya Taifa Stars kwa kuwa itaweka kambi hapa
Nchini kwa muda wa wiki moja kuanzia Februari 18 hadi 25 kwa ajili ya
kujiandaa na mechi yao ya mchujo ya kuwania kushiriki Fainali za Kombe
la Afrika (CAN) dhidi ya Mauritius.
Ofisa Habari wa Shirikisho la
Soka Tanzania, Boniface Wambura alisema kuwa mechi ya DRC na Mauritius
itachezwa Februari 29, nchini Mauritius, huku Stars yenyewe itacheza
mechi ya kwanza ya mchujo kwa ajili ya fainali hizo za Kombe la Afrika
(CAN) 2013 zitakazofanyika Afrika Kusini dhidi ya Msumbiji.
Alisema kutokana na timu ya
Misri kuomba kucheza na Stars tarehe kama hizo wanafanya mawasiliano na
Misri kuona kama wanaweza kusogeza mbele au kurudisha nyuma na kama
haitawezekana wapeleke timu ya vijana kucheza na Misri.
"Tuna mashindano makubwa mbele
yetu tunahitaji mechi nyingi za kirafiki hivyo hatutaki kuzikosa,
tutaongea na Misri kama wanaweza wasogeze mbele au warudishe nyuma
ikishindikana kabisa tutawaomba tupeleke timu ya vijana," alisema
Wambura.
Mwezi Mei, 2009 Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo (DRC) ambao walikuwa mabingwa wa Afrika wa
michuano ya wachezaji wa ligi za ndani (CHAN) ambazo pia Tanzania
ilishiriki, walicheza mechi ya kirafiki ya kimataifa na Taifa Stars na
kuilaza mabao 2-0 katika uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Walikuwa DRC ambao walikuwa wa
kwanza kupata bao katika dakika ya tano, lililofungwa na Kaluyituka
Dioko baada ya mabeki wa Stars kujichanganya katika kuokoa mpira wa
kona. Katika kipindi cha pili Kaluyituka aliwaduwaza tena Watanzania
kwa kufunga bao la pili.
Katika viwango vya Shirikisho
la Soka Kimataifa FIFA, timu ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC)
inashika nafasi ya 125 huku Tanzania ikishika nafasi ya 137.
Kihistoria DRC ndiyo timu ya
kwanza katika Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara kufuzu kushiriki
Fainali za Kombe la Dunia 1974, na pia imewahi kutwaa ubingwa wa Kombe
la Afrika (CAN) mara mbili, ambapo mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1968 na
mara ya pili mwaka 1974.
DRC inaundwa na nyota wengi
wanaotokea katika klabu ya TP Mazembe kama Miala Nkulukutu, Joel
Kimwaki, Bedi Mbenza, Eric Bokanga na Tresor Mputu, kinanolewa na kocha
Claude Le Roy.
Kocha wa Taifa Stars, Jan
Poulsen anatakiwa kuhakikisha kikosi chake kinapata ushindi katika
mechi hiyo ili kuweza kurudisha imani kwa mashabiki wa soka wa Tanzania
ambao wanaipenda Taifa Stars ila imekuwa ikiwakitisha tamaa mara kwa
mara.
Taifa Stars imewahi kushiriki
mara moja Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN) mwaka 1980, lakini haijawahi
kushiriki fainali za Kombe la Dunia na imekuwa ikitolewa katika hatua
za awali katika harakati zote za kufuzu
michuano hiyo.
Source:Mwananchi
No comments:
Post a Comment