1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge kanuni ya 99(7), toleo la mwaka
2007 na kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,napenda kuwasilisha
maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi
ya Mafungu ya Wizara ya Fedha – Fungu 50 Wizara ya Fedha, Fungu 21
Hazina, Fungu 22 Deni la Taifa na Fungu 23 Ofisi ya Mhasibu Mkuu wa
Serikali. Vile vile Fungu 10 Tume ya Pamoja ya Fedha na Fungu 13 Kitengo
cha Udhibiti wa Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi.
Mheshimiwa
Spika, mafungu yote yaliyo chini ya Wizara ya Fedha yanaomba
kuidhinishiwa na Bunge lako tukufu jumla ya shilingi Bilioni 4,208
(trilioni 4.2) ili yaweze kutekeleza majukumu yake. Mafungu haya maombi
yake ya Fedha ni sawa na asilimia 28 ya Bajeti nzima ya Serikali ya
mwaka wa Fedha 2012/13.
Mheshimiwa
Spika, Wizara ya Fedha ndiyo msimamizi mkuu wa Uchumi wa nchi
ikitekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo, kusimamia ukusanyaji wa mapato
ya ndani na ya nje, kusimamia matumizi ya Serikali, kusimamia utendaji
wa Taasisi na Mashirika ya Umma, kusimamia manunuzi ya Serikali na
Taasisi na Mashirika ya Umma, kusimamia Deni la Taifa na dhamana za
Serikali, kutafuta suluhisho na kusimamia mfumo wa kodi wa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano na kupambana na Fedha haramu.
Sambamba na hayo ni kusimamia na kutekeleza mpango wa kupunguza umasikini nchini kupitia utekelezaji wa MKUKUTA II.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha na mafungu yote yaliyo chini yake ndio
moyo wa Serikali na hivyo ni lazima kuitazama Wizara hii kwa jicho kali
na kutilia mashaka kila jambo ambalo inalifanya ili kuhakikisha kuwa
moyo huu hausimami maana madhara yake ni kwa taifa zima na watu wake.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kupitia Waziri Kivuli wa Fedha
inatekeleza wajibu huu kwa Uzalendo, Uadilifu na kwa misingi ya
Uwajibikaji. Tumetekeleza wajibu huu na tunaendelea kuutekeleza bila
kujali maneno na kuweka maslahi ya Taifa letu mbele ya kila kitu
kingine. Maslahi ya Taifa ni zaidi ya vyama vya siasa, mahala tunapotoka
au dini tunazoamini. Maslahi ya Taifa ni kwa ajili ya Watazania na hasa
Watanzania milioni 30 (The Bottom 30M) ambao bado wanaishi katika
ufukara mkubwa sana wakikosa huduma muhimu za jamii na wanaoishi
vijijini ambapo hakuna umeme, barabara hazipitiki na wanahangaika kutwa
kutafuta maji safi na salama. Maslahi ya Taifa sio faida ya wachache
wenye kuishi mijini au wanasiasa wanaotafuta ushawishi kwa umma bila
kujali matakwa ya Umma. Watanzania wanyonge wa vijijini wanajua maslahi
yao ni nini. Wanajua kina nani wanapigania maslahi ya Wanyonge.
2.0 MAPATO YA SERIKALI
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya mwenendo wa Uchumi ya mwezi
Julai (Monthly Economic Review, July 2012) iliyotolewa na Benki Kuu ya
Tanzania, katika kipindi cha mwezi Juni Serikali iliweza kukusanya kiasi
cha shilingi bilioni 998.0. Hata hivyo matumizi halisi yalikuwa kiasi
cha shilingi bilioni 1,911.8 hali iliyopelekea kuwepo kwa nakisi baada
ya kuondoa msaada wa masharti wa masharti wa shilingi bilioni 400.2;
nakisi hiyo ililipwa kwa vyanzo vya ndani na nje.
Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo ilionyesha kuwa mapato yote ukiondoa
fedha zilizokusanywa na Serikali za mitaa kwa mwezi Juni, yalikuwa kiasi
cha shilingi bilioni 887.5 ambacho ni zaidi ya asilimia 38.1 ya malengo
yaliyokuwa yamewekwa kukusanywa mwezi huo. Aidha, Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) ilikusanya kiasi cha shilingi bilioni 753.3, kiasi
ambacho ni zaidi ya asilimia 22.3 ya malengo ya makusanyo kilichokuwa
kimewekwa na mamlaka hiyo. Makusanyo haya ni makubwa zaidi kukusanywa na
TRA kwa mwezi mmoja tangu Mamlaka hiyo ianzishwe.
Mheshimiwa Spika, katika makusanyo hayo ya mwezi Juni Mamlaka ya Mapato
Tanzania ilikuwa imejiwekea lengo la kukusanya kiasi cha shilingi
bilioni 242.4 kama kodi ya Mapato, lakini ilikusanya kiasi cha shilingi
bilioni 366.0 kiasi ambacho ni zaidi kwa asilimia 60.8 ya malengo
yaliyokuwa yamewekwa.
2.0 MAPATO YA SERIKALI
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya mwenendo wa Uchumi ya mwezi
Julai (Monthly Economic Review, July 2012) iliyotolewa na Benki Kuu ya
Tanzania, katika kipindi cha mwezi Juni Serikali iliweza kukusanya kiasi
cha shilingi bilioni 998.0. Hata hivyo matumizi halisi yalikuwa kiasi
cha shilingi bilioni 1,911.8 hali iliyopelekea kuwepo kwa nakisi baada
ya kuondoa msaada wa masharti wa masharti wa shilingi bilioni 400.2;
nakisi hiyo ililipwa kwa vyanzo vya ndani na nje.
Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo ilionyesha kuwa mapato yote ukiondoa
fedha zilizokusanywa na Serikali za mitaa kwa mwezi Juni, yalikuwa kiasi
cha shilingi bilioni 887.5 ambacho ni zaidi ya asilimia 38.1 ya malengo
yaliyokuwa yamewekwa kukusanywa mwezi huo. Aidha, Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) ilikusanya kiasi cha shilingi bilioni 753.3, kiasi
ambacho ni zaidi ya asilimia 22.3 ya malengo ya makusanyo kilichokuwa
kimewekwa na mamlaka hiyo. Makusanyo haya ni makubwa zaidi kukusanywa na
TRA kwa mwezi mmoja tangu Mamlaka hiyo ianzishwe.
Mheshimiwa Spika, katika makusanyo hayo ya mwezi Juni Mamlaka ya Mapato
Tanzania ilikuwa imejiwekea lengo la kukusanya kiasi cha shilingi
bilioni 242.4 kama kodi ya Mapato, lakini ilikusanya kiasi cha shilingi
bilioni 366.0 kiasi ambacho ni zaidi kwa asilimia 60.8 ya malengo
yaliyokuwa yamewekwa kutokana na kuongezeka kwa bei ya mauzo ya dhahabu.
Hata hivyo Manunuzi yetu kutoka nje yamefikia dola za Kimarekani 12,959
milioni.
Mheshimiwa
Spika, taarifa hiyo inaonyesha kuwa mauzo ya dhahabu Nje kwa mwaka 2011
yalikuwa kiasi cha dola 2,330.7 milioni sawa na aslimia 56.7% ya mauzo
yote nje, wakati mauzo ya nje kutokana na bidhaa zilizozalishwa
viwandani yalikuwa na jumla ya dola 922.0 milioni sawa na asilimia 22.4%
ya mauzo yote ya nje. Aidha mauzo ya mazao mbalimbali kama Pamba,
Katani, Korosho, Chai, Kahawa na mengineyo yalikuwa na thamani ya dola
761.1 milioni kwa kipindi hicho cha mwaka 2012.
Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo imeendelea kuonyesha kuwa tuliagiza
bidhaa kutoka nje zenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 12,958.7.
Katika manunuzi hayo tuliyofanya mafuta peke yake yalikuwa na thamani ya
dola za Kimarekani milioni 3,586.1 ambalo ni ongezeko la asilimia
60.08% ukilinganisha na kipindi kama hicho kwa mwaka 2011.
Mheshimiwa Spika, takwimu hizi zinaonyesha kwamba fedha zote za kigeni
zilizotokana na mauzo ya dhahabu, bidhaa za viwandani na Korosho
zilitumika kuagiza mafuta pekee yake! Hali hii ni mbaya sana kwa uchumi
wa Taifa letu na juhudi zote za kuongeza mauzo nje zinaliwa na uagizaji
wa Mafuta ambao umepanda sana katika siku za hivi karibuni.
6
Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua kuwa kuanzia mwaka jana Serikali
imekuwa ikitekeleza mpango wa Umeme wa dharura ambao umepelekea matumizi
makubwa ya Mafuta. Hata hivyo ieleweke kuwa Mpango mzima wa Manunuzi ya
Mafuta ya kuendesha mitambo ya Umeme inaligharimu Taifa Fedha nyingi
sana. Takwimu zinaonyesha kuwa Serikali inapaswa kutumia zaidi ya
shilingi 42 bilioni kila Mwezi kuendesha mitambo ya dharura ya Umeme.
Manunuzi yenyewe ya Mafuta yamejaa mazonge ya ufisadi uliokithiri.
Licha ya kutaka Spika aunde timu ya kuchunguza ufisadi katika manunuzi
ya Mafuta na licha ya Kamati ya Bunge kutaka Uchunguzi wa kibunge
kufanyika katika manunuzi haya bado hakuna hatua inayochukuliwa. Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Mamlaka ya Manunuzi ya Umma PPRA kufanya
uchunguzi wa kina kuhusu manunuzi ya mafuta kuzalisha Umeme ambayo
yanachoma bilioni 42 za Serikali kila Mwezi. PPRA hapaswi kufumbia macho
manunuzi yanayotafuna shilingi 1.4 bilioni kila siku na yanayoongeza
manunuzi ya nchi kutoka nje (imports) na hivyo kupoteza fedha za kigeni
hovyo.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha ambayo ndio wizara mama ya PPRA
kupitia Fungu 50, na ndio Wizara yenye kusimamia uchumi wa nchi kwa
ujumla ituletee Bungeni Taarifa ya Uchunguzi utakaofanywa na PPRA kuhusu
manunuzi shilingi 1.4 bilioni kila siku ya mafuta kuendesha mitambo ya
kuzalisha Umeme.
2.3 Deni la Taifa.
Mheshimiwa Spika, Fungu 22 linaombewa jumla ya shilingi bilioni 2,735
ili kuweza kulipa madeni ikiwemo deni la nje la shilingi bilioni 373 na
trilioni 1.5 kama deni la ndani. Kwa mujibu wa taarifa ya mwenendo wa
uchumi ya mwezi Julai 2012, deni la nje la Taifa (external debt) mpaka
mwisho wa mwezi Juni 2012 lilikuwa limefikia kiasi cha dola za
Kimarekani milioni 10,354.6 kiasi ambacho ni ongezeko la zaidi ya dola
milioni 385.9 kwa kipindi kama hicho mwaka 2011. Aidha katika kipindi
hicho deni la ndani lilikuwa kiasi cha shilingi bilioni 4,174.2. Kambi
ya Upinzani Bungeni ina taarifa kwamba takwimu hizi za Deni la Taifa
hazihusishi dhamana ambazo Serikali imezitoa kwa Mashirika ya Umma na
Kampuni binafsi.
Dhamana
lazima katika siku za usoni ziwe ni sehemu ya deni la Taifa maana
tumeshuhudia sasa ambapo Kampuni nyingi binafsi zimeshindwa kulipa
mikopo iliyodhaminiwa na Serikali. Mfano ni malipo ya deni lenye thamani
ya shilingi bilioni 60 la kukodisha ndege ya Airbus kwa Shirika la ATCL
kutoka kampuni ya Wallis Traders ya Lebanon na Deni lililochukuliwa na
Kampuni ya Kiwira Coal and Power limited ambayo mbia wake alishindwa
kuendesha mradi wa Makaa ya Mawe Kiwira licha ya kudhaminiwa na Serikali
Mkopo kutoka kwenye taasisi za Fedha hapa nchini ambapo sasa Serikali
imepanga kulipa shilingi bilioni 40 katika Bajeti ya mwaka huu.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani haina tatizo na uhimilivu wa Deni la
Taifa (Debt sustainability) kwani tunajua kuwa mataifa makubwa yanakopa
sana na yana uwiano mkubwa wa Deni kwa GDP kuliko sisi. Tatizo letu ni
namna ambavyo fedha za mikopo zinatumika. Matumizi ya mikopo
tunayochukua sio endelevu maana sehemu ya mikopo hiyo hutumika kwa
matumizi ya kawaida badala ya matumizi ya uzalishaji au kuongeza uwezo
wetu wa kuzalisha.
Kambi Rasmi ya Upinzani inaendeleza wito wake wa kutaka Fungu 22 la deni
la Taifa lifanyiwe ukaguzi maalum (Special Audit) ili tuweze kujua
mikopo hii tunayochukua kila wakati inatumika kufanyia nini? Miradi
iliyotekelezwa kutokana na Madeni ambayo Waziri wa Fedha aliitangaza
wakati wa kufunga mjadala wa Bajeti kuu ya Serikali ifanyiwe ukaguzi
kutambua ukweli na kuona thamani ya Fedha.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaendelea kuhoji kama
tulivyohoji mwaka 2011/2012 kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma.
Katika fungu 21, kasma 229929, Serikali imetenga Shilingi bilioni 26.4
kwa ajili ya kulipa fidia kwa mikataba mbalimbali ambayo Serikali
imeingia. Hii inaonyesha kuwa Serikali inatumia fedha nyingi sana kwa
ajili ya mikataba iliyoingiwa na Mashirika ya Umma na kuliletea hasara
Taifa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani pamoja na kutaka majibu kutoka
kwa serikali, bado tunataka kuwe na usimamizi thabiti ili kulinda fedha
za umma zinazotumika kwenye Mashirika ya Umma, ambapo kumekuwa na
usimamizi mbovu sana na unaopelekea Taifa kupoteza fedha nyingi sana
kutokana na ubadhirifu katika Mashirika ya Umma. Hii ni kweli kwa
Mashirika ambayo Serikali inamiliki sehemu ya hisa.
2.5 MKOPO WA KUNUNUA RADA ILIYOGUBIKWA NA UFISADI
Mheshimiwa Spika, sehemu ya Malipo ya Deni la Taifa ni Mkopo ambao
Serikali ilichukua ili kununua Rada kutoka kampuni ya BAE ya Uingereza.
Suala hili la rada limejadiliwa sana nchini kwa upande mmoja tu wa
ufisadi wa kupandisha bei ya Rada na hatimaye kurejeshwa kwa iliyoitwa
chenji ya Rada. Hiyo ilikuwa ni nusu tu ya ukweli kuhusu suala la Rada
kwani Serikali ilikopa kiasi cha dola za kimarekani 40 milioni kutoka
Benki ya Barclays ya Uingereza kwa ajili ya kununulia Rada. Mkopo huo
ulikuwa na Riba ya asilimia 4.9 juu ya kiwango cha riba zinazotolewa na
Benki ya Dunia au IMF.
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua kama mkopo huu umeshalipwa wote na
jumla tulilipa kiasi gani cha fedha. Ukilinganisha fedha iliyorejeshwa
kama chenji ya Rada na Fedha ambayo Tanzania iliilipa Benki ya Barclays
(Principal amount na Interest), je chenji ya Rada ilikuwa na thamani
yoyote kifedha? Mjadala wa ununuzi wa Rada hauwezi kuisha kwa kufurahia
kurejeshewa chenji tu. Mjadala huu bado mbichi kabisa kwani tunataka
ukweli na ukweli mtupu uelezwe kwa umma na kuona Taifa lilipata hasara
kiasi gani kwa ufisadi huu wa kimataifa na hatua stahiki za kisheria
kuchukuliwa dhidi ya wote walioingiza hasara kwa Taifa letu.
2.4 Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu
Mheshimiwa Spika, taifa letu limekuwa na sheria nyingi ambazo ziliwahi
kutungwa kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la fedha haramu, rushwa na
uhalifu uliopangwa hapa nchini mwetu tangu tupate uhuru na hii
inathibitishwa na uwepo wa sheria zaidi ya 15 kuwahi kutungwa tangu
uhuru (tazama kiambatanisho A). Vile vile Bunge liliimarisha Sheria ya
Udhibiti wa Fedha Haramu mwaka 2011. Hata hivyo bado nchi yetu
imegubikwa na fedha chafu na hasa wizi katika Mabenki hapa nchini.
Wakati sheria ya Fedha haramu inayataka Mabenki kutunza kumbukumbu
sahihi za wateja, kumekuwa na matukio (yaliyoripotiwa na yasiyoripotiwa)
ya Wafanyakazi wa mabenki hapa nchini kushirikiana na baadhi ya
wananchi kuiba fedha za wateja na hasa wateja ambao wamefariki dunia na
ndugu na jamaa zao kutojua taarifa za kibenki za marehemu hawa.
Serikali inapaswa kufahamu kuwa wizi kwenye mabenki ni moja ya sifa
mbaya sana ya mfumo wetu wa fedha na hivyo kusababisha Benki kuweka riba
kubwa sana ili kufidia ‘risk’ kama hizi za watu ‘kupiga’ amana za
wateja kwenye mabenki. Kambi Rasmi ya upinzani inaitaka Wizara ya Fedha
kupitia Kitengo cha Udhibiti wa Fedha haramu kudhibiti wizi kwenye Benki
za hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kupata maelezo ya kina
juu ya matatizo ya mtaji “Capital under pressure” yanayoikabili benki
ya NBC na hatua zilizochukuliwa na Serikali kama mmoja wa wanahisa dhidi
ya mwanahisa mwenye dhamana ya kuisimamia Benki hiyo (ABSA) kwa
kushindwa kuisimamia kwa umakini na hivyo kuiingiza katika matatizo hayo
ya mtaji. Mheshimiwa Spika, hivi sasa wanahisa (ambapo Serikali ni
mmoja wao) wanapaswa kuongeza mtaji katika benki ya NBC ili kuinusuru,
Benki ambayo ni moja ya Benki kubwa kabisa hapa nchini ambayo kama
ingekuwa na usimamizi mzuri ingepaswa kujiendesha yenyewe na kutoa gawio
kwa wanahisa.
Mheshimiwa
Spika, taarifa iliyotolewa na Benki Kuu ya Uswissi na kuchapishwa na
magazeti mbalimbali ya hapa nchini mwezi June, 2012 inanonyesha kuwa
viongozi wa Serikali pamoja na wafanyabiashara wakubwa wametorosha fedha
zao katika mabenki ya Uswissi kiasi cha shilingi bilioni 315.5. Habari
zaidi zinaeleza kwamba mabilioni haya yanatokana na ‘deals’ zilizofanywa
na watendaji wa Serikali na wafanyabiashara kadhaa kwenye sekta za
Nishati na Madini. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imepata taarifa kuwa
mmoja wa Viongozi wa juu kabisa wa Tanzania na baadhi ya Mawaziri wa
Serikali za awamu zilizopita ni miongoni mwa wamiliki wa Fedha hizi.
Sehemu kubwa ya Fedha zililipwa na Kampuni za utafutaji wa Mafuta na
Gesi katika Pwani ya Mkoa wa Mtwara zilizopewa mikataba kati ya mwaka
2004 na 2006. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa taarifa
rasmi ya hatua gani imechukua mara baada ya taarifa ile kutoka Benki ya
Taifa ya Uswissi ilipotolewa. Tunaitaka Serikali kuliambia Taifa hatua
itakazochukua kurejesha fedha hizi na nyingine zozote ambazo zimefichwa
ughaibuni. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni italazimika kuweka wazi
taarifa na majina ya watu wenye umiliki wa fedha katika Benki za nchini
Uswissi iwapo Serikali haitatoa taarifa rasmi kuhusu suala hili.
Mheshimiwa Spika, Aidha, kuna taarifa nyingine zinaonyesha jinsi ambavyo
taifa linaibiwa kupitia kesi mbalimbali ambazo Serikali imeshitaki au
kushitakiwa kwenye Mahakama za Kimataifa. Mfano mzuri ni Kesi ya IPTL na
Standard Chartered Bank ya Hong Kong ambayo imechukua muda mrefu bila
kuisha na kuliingizia taifa hasara kubwa sana. Tunapenda kufahamu ni kwa
nini mpango wa kumaliza kesi hii nje ya Mahakama hautekelezwi na vile
vile mpango wa kugeuza Mtambo wa kufua umeme wa IPTL kuwa wa Gesi kwa
nini hautekelezwi?
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kupata majibu kuhusu mambo yafuatayo;
Kwanza,
fedha zilizoko kwenye Escrow Akaunti Benki Kuu za IPTL (Tegeta escrow)
zimefikia kiasi gani mpaka sasa, na usalama wa fedha hizo ukoje?
Ikumbukwe kwamba kuna uamuzi wa Bunge kwamba Fedha hizi zisitumike wala
kutolewa mpaka maamuzi kuhusu mtambo wa IPTL kufikiwa na hasa uamuzi wa
kugeuza mtambo huu kutumia Gesi Asilia.
Pili, Suala hili la kesi ya IPTL limechukua muda mrefu sana na sasa ni
wakati muafaka likamalizwa nje ya mahakama kwa Waziri wa Fedha kukutana
na pande zote za mgogoro huu ili liweze kufikia mwisho.
2.6 Kampuni ya Oxford University Press Tanzania Kufungiwa Mheshimiwa
Spika, mnamo tarehe 03 Julai 2012 Benki ya Dunia ilitangaza kuifungia
kampuni ya uchapishaji ya Oxford University Press Tanzania Ltd (OUPTL)
kutokana na vitendo vya rushwa ambavyo kampuni hiyo ilikiri kuhusika
kwake kwenye miradi mbalimbali ya elimu iliyokuwa inafadhiliwa na Benki
hiyo katika ukanda wa Afrika Mashariki. Mheshimiwa Spika, kampuni hiyo
ilikiri kuhusika katika kuwahonga maafisa mbalimbali wa Serikali katika
mkataba wake wa kusambaza vitabu na kampuni hiyo ilikubali kuilipa Benki
ya Dunia kiasi cha dola 500,000 kama sehemu ya makubaliano yake
kutokana na kashfa hiyo.
Mheshimiwa
Spika, mamlaka ya manunuzi ya umma ilitangaza kuifungia kampuni hiyo
hapa nchini kwa kipindi cha miaka saba, wakati ambao tayari tulishawapa
zabuni ya kusambaza vitabu vilivyotokana na chenji ya rushwa ya Rada
ambazo ziliamuliwa kuwa zitaenda kununua vitabu. Kambi Rasmi ya Upinzani
inaitaka Serikali kuinyang’anya kampuni hii zabuni ya kuchapisha na
kusambaza vitabu hivyo na badala yake kazi hiyo yapewe makampuni ya
ndani ya nchi. Tabia ya Serikali kufanya kazi na Kampuni ambazo tayari
zina dosari ama za kifisadi au kukiuka sheria na maagizo ya Serikali
inatoa picha mbaya kwenye uchumi. Hali kadhalika, Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali kuwachukulia hatua maafisa wote wa Wizara
waliohusika katika “rushwa ya Oxford”.
3.0 Mishahara hewa nchini
Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya
Upinzani kuhusu makadirio ya mapato na matumizi katika Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa mwaka wa fedha 2012/2013, tulitaja
kiasi cha shilingi bilioni 91 ambazo zililipwa kama mishahara kwa
watumishi hewa kama ilivyoripotiwa na magazeti ya ‘The Daily News’ na
‘The Guardian’ ya Machi 23, 2011.
Mheshimiwa
Spika, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya
tarehe 31 Machi, 2012 inaonesha kwamba kwa mwaka wa fedha 2010/2011
jumla ya shilingi 142,715,827.992 zililipwa kama mishahara kwa wastaafu,
watumishi walioacha au kufukuzwa kazi na watumishi wengine ambao
hawakustahili. Aidha, ripoti hiyo imeonesha kiasi cha shilingi
1,842,607,565.29 zilizolipwa kama mishahara hewa kwa mwaka wa fedha
2009/2010.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Fedha kwa kamati ya
kudumu ya Bunge ya fedha na uchumi ya tarehe 7 Agosti, 2012 ni kwamba
uhakiki wa watumishi uliofanyika mwezi Januari, 2012 kwenye Halimashauri
133 na kwenye taasisi na wakala za Serikali 154 ulibaini majina 9,949
ya watumishi wasiostahili kuwemo kwenye orodha ya mishahara. Idadi hii
ya watumishi hewa ni sawasawa na takribani idadi ya watumishi
walioajiriwa katika sekta nzima ya madini kwenye migodi ya dhahabu hapa
nchini. Watumishi hewa wanaokaribia 10,000 ni wengi mno na inaonyesha
dhahiri namna Serikali isivyo makini katika suala hili ambalo
linasababisha upotevu mkubwa wa Fedha za Umma.
Mheshimiwa Spika, Waziri wa Fedha alikiri mbele ya Kamati ya Fedha na
Uchumi kwamba mwezi Februari Serikali ililipa shilingi bilioni 5.1 kama
mishahara hewa. Hii maana yake ni kwamba Serikali
2 Tazama Ripoti ya CAG toleo la Kiingereza uk.37.hutumia zaidi ya shilingi bilioni 70 kila mwaka kwa watumishi hewa wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, tunataka fedha hizi wanazolipwa watumishi hewa
zitumike kuwalipa walimu na madaktari madai yao kwani ni nyingi na
zinatosha sana. Siku zote sababu za Serikali kutotimiza matakwa ya
wafanyakazi kwenye sekta ya Afya na Elimu ni kwamba Serikali haina
Fedha. Lakini hapa tunashuhudia Shilingi bilioni 70 kila mwaka
zikiteketea kulipa watumishi hewa ambao hawapo, hawafanyi kazi na hivyo
kufaidisha mtandao wa kifisadi ambao kwa vyovyote vile unaanzia Wizara
ya Fedha na Wizara ya Utumishi. Serikali inakosa vipi fedha za kulipa
madai ya Walimu na inapata za kulipa watumishi hewa? Serikali inakosa
vipi fedha za kulipa Madaktari na Manesi lakini inapata shilingi bilioni
70 kila mwaka kulipa watumishi hewa?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka mradi huu wa watumishi
hewa wenye mauzo (turnover) ya shilingi 70 bilioni kwa mwaka
uvunjwevunjwe ili kupata fedha za kulipa Walimu na Madaktari. Waziri wa
Fedha asambaratishe mtandao huu mwovu ambao sasa umeota mizizi kwenye
Taasisi za Serikali. Vile vile Waziri agawe kwa Wabunge taarifa ya
uhakiki wa wafanyakazi wa Serikali na pia hatua ambazo Serikali
imechukua dhidi ya vinara wa mtandao wa watumishi hewa Serikalini.
4.0 Benki Kuu ya Tanzania-(BOT)
Mheshimiwa
Spika, taasisi hii ndiyo yenye dhamana ya kutayarisha na kusimamia sera
za fedha na utendaji mzima wa taasisi za fedha kwa ujumla. Katika
kutekeleza hilo Benki Kuu ndicho chombo kinachoweka miongozo kwa taasisi
za fedha, taasisi za bima na taasisi za hifadhi za jamii ili
kuhakikisha fedha za wanachama katika taasisi hizo zinalindwa.
Mheshimiwa Spika, taasisi za fedha zimegawanyika katika sehemu kuu
mbili, ambazo ni tasnia ya benki (Banking industry) na tasnia ndogo ya
fedha (Microfinance industry). Tasnia zote hizi zinahudumia wateja
tofauti kwa kulingana na wanachojishughulisha nacho katika kuinua kipato
cha familia inayomtegemea, mteja yuko kwenye sekta binafsi au sekta
rasmi ya ajira.
Mheshimiwa Spika, Benki Kuu katika kutimiza wajibu wake inailazimu kutoa
vigezo vitakavyozingatiwa katika utoaji wa mikopo ili kukabiliana na
wakopaji ambao wanaweza kuwa na lengo la kuchukua fedha wakati hawana
nia ya dhati ya kurejesha mikopo yao.
4.1 RIBA KATIKA TAASISI ZA FEDHA
Mheshimiwa Spika, tofauti kati ya viwango vya riba vinavyotozwa kwenye
mikopo na vile vinavyotolewa kwenye amana kama faida vimeendelea kuwa
juu, licha ya kuongezeka kwa ushindani katika sekta ya kibenki. Hii
imechangiwa kwa kiasi kikubwa na kukosekana kwa taarifa sahihi za
wakopaji (credit reference data bank) na kutokuwepo kwa taasisi ya
utoaji wa taarifa sahihi za waombaji mikopo (Credit Rerefence Bureau)
nchini. Aidha, gharama kubwa za kufanya biashara kutokana na miundombinu
hafifu, nazo zimechangia kuongeza viwango vya riba vinavyotozwa kwenye
mikopo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaomba taarifa ya kuanzishwa
kwa Credit Reference Bureaux kwa mujibu wa Sheria ya Benki na Taasisi za
Fedha ya mwaka 2006.
4.2 Usimamizi Wa Tasnia Ndogo ya Fedha (Microfinance Industry-MFI)
Mheshimiwa Spika, tasnia hii ndiyo inayoshughulika moja kwa moja na
kundi kubwa la Watanzania ambao hawako kwenye mfumo rasmi wa ajira kwa
kuwapa mikopo midogo midogo kwa shughuli rasmi au zisizo rasmi, ili
kuhakikisha kuwa kipato cha familia kinapanda na hivyo uchumi wa
mwananchi mmoja mmoja unakua.
Mheshimiwa Spika, tasnia hii inalenga kuboresha maisha ya wananchi wa
vijijini na maeneo mbalimbali ya mijini. Tasnia hii inalenga kuboresha
maisha kwa wananchi mmoja mmoja au makundi (Saccoss) na benki jamii
(vicoba) ambazo zimekuwa na wanachama wengi wanaoendelea kujiunga ili
kujikwamua kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, kukosekana kwa mdhibiti anayeelewa jinsi tasnia hii
inavyofanya kazi zake na aina ya wateja inaowahudumia ni udhaifu mkubwa
unaosababisha tasnia hii kushindwa kukua. Kukosekana kwa udhibiti wa
sekta ndogo ya Fedha kunasababisha wananchi masikini kuumia sana. Mfano
tumeshuhudia namna Kampuni za kukopesha zinavyowafanya Walimu vijijini
kuwa masikini zaidi kwa kuweka riba kubwa sana. Hata hivyo Serikali
imekaa kimya bila kusaidia wanyonge hawa kwa kuchukua hatua madhubuti za
kudhibiti na kusimamia sekta hii. Mfano mzuri wa Serikali kushindwa
kusaidia wanyonge ni pale ambapo wannachi wengi sana kujikuta wamepoteza
fedha zao kupitia ‘schemes’ kama vile DECI ambapo wananchi walikusanya
zaidi ya shilingi bilioni 16 ambazo mpaka sasa hata riba yake hatujui
inakwenda wapi?
Kungekuwa na Mamlaka ya kusimamia sekta ya fedha kwa ajili ya wanyonge tusingeshuhudia unyonyaji huu.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuunda
Mamlaka ya Usimamizi wa sekta ndogo ya Fedha (Tanzania Microfinace
Regulatory Authority) hapa nchini badala ya Benki Kuu ya Tanzania ambayo
ndiyo msimamizi wa tasnia ya benki. Lengo ni kuhakikisha kuwa wananchi
wa vijijini wanaopata mikopo kutoka kwenye taasisi za Benki wanalindwa
na dola. Mamlaka italinda Haki za wanyonge dhidi ya ‘loan sharks’ na
Wajibu wa wanyonge wenye kuchukua mikopo.
Mheshimiwa Spika, kuundwa kwa chombo chenye mamlaka ya kusimamia taasisi
ndogo ya fedha ni lazima kutokana na ukweli kwamba kuna utofauti wa
muundo baina ya mabenki na taasisi ndogondogo za fedha; inakuwa ni
vigumu kudhibiti riba na utoaji wa vigezo vya kifedha katika kuhudumia
wananchi na kutoa mikopo kwa wateja wa tasnia hizo mbili zilizo tofauti
kimuundo.
Mheshimiwa Spika, kuwepo kwa chombo chenye mamlaka pia itasaidia kuwa na
Credit Reference Bureau itakalokuwa na taarifa za wakopaji kutoka
taasisi ndogondogo za fedha tofauti na itakayosimamia wadaiwa wa mabenki
na taarifa hizi zitasaidia udhibiti wa wateja wa taasisi hizi kuchukua
zaidi ya mkopo mmoja kwenye taasisi tofauti tofauti ambapo hali hii
husababishwa na ucheleweshaji wa mikopo inayotolewa na taasisi hizi
pamoja na uhafifu wa mikopo katika kumsaidia mlengwa.
4.3 Mifuko ya Hifadhi za Jamii
Mheshimiwa Spika, Mifuko ya Hifadhi za Jamii ni mojawapo ya sekta ambayo
ina uwezo mkubwa wa kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana wetu, kama
uwekezaji unaofanywa kwa kutumia mifuko hiyo utasimamiwa vizuri.
Meshimiwa Spika, inaonesha kwamba mifuko hii imekuwa ikikusanya michango
ya wanachama na kulipa wastaafu wanachama wa Mifuko hii vizuri.
Kutokana na maelekezo ya sheria mpya iliyoleta mjadala baina ya
wafanyakazi na serikali juu ya mabadiliko ya sheria na utoaji wa mafao
kwa wafanyakazi, pamoja na Bunge
21
kutaka mabadiliko ya sheria hiyo bado kuna haja ya kutazama namna mifuko ifanyavyo kazi.
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuweka wazi utendaji wa Mifuko
hii katika maeneo nyeti yafuatayo, kwanza Ukwasi wake (Liquidity of the
Social Security funds), pili Uwekezaji (Investments) pia Risk
Management reports. Taarifa katika maeneo haya hupelekwa na mifuko
kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma na kutokana na
utaratibu wa Kazi wa Kamati hii ya POAC ni vigumu wananchi wote kuona
taarifa hizi ambazo ni muhimu kuwa wazi kwa umma. Taarifa kama hizi
zitaliwezesha Bunge kuelewa kiwango cha usalama wa Mifuko hii na uwezo
ziada (excess financial capacity) kuendelea kutoa huduma zinazohitajika.
Kama ilivyo kwa Mabenki, tunashauri kuwa taarifa za robo mwaka za
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ziwe zinatangazwa kwenye magazeti yanayosomwa
zaidi nchini ili wananchi na hasa wanachama wa mifuko waone namna
mifuko yao inavyofanya kazi.
Mheshimiwa Spika, aidha, kwa kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani kwa kipindi
chote imekuwa ikitoa ushauri katika sekta hii, hatuna budi kurudia
ushauri tulioutoa mwaka jana kama ifuatavyo:
“Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapendekeza kwa Mifuko ya PSPF na
PPF kuangalia namna ya kuwekeza katika maeneo yanayochochea ukuaji wa
uchumi na hivyo kuzalisha ajira na kupata wanachama zaidi. Maeneo kama
uwekezaji kwenye Bandari na Reli yanapaswa kuangaliwa kwani kutokana na
Jiografia ya nchi yetu ni maeneo yanayoweza kuzalisha faida kubwa sana.
Tunaitaka Serikali ilieleze Bunge kuna mipango gani katika Mashirika
haya (PSPF na PPF) kuangalia maeneo mapya ya uwekezaji katika
miundombinu na hasa Bandari.
Mheshimiwa Spika, Mifuko ya hifadhi ya jamii imewekeza katika miradi ya
ujenzi wa nyumba nafuu kwa ajili ya wanachama wao na pia wanachi kwa
ujumla. Tunasisitiza Miradi hii isiwe Dar es salaam na Mwanza tu bali
ienee nchi nzima kama ambavyo mfuko wa PSPF umeanza.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani pia inashauri kwamba fao la Elimu
ambalo Mfuko wa PPF unatoa kwanza litolewe na Mifuko mingine pia lakini
pia lipanuliwe hadi kufikia elimu ya Chuo Kikuu. Fao hili la Elimu
ambalo ni muhimu sana na twapongeza mfuko wa PPF kwa kulianzisha ni fao
ambalo litasaidia sana kuhakikisha kuwa yatima ambao wazazi wao wanakuwa
wamefariki wanapata uhakika wa kuendelea na masomo. Fao hili liwe fao
la lazima kwa mifuko yote nchini.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni bado inasisitiza ushauri
wake kuwa Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii ihamishiwe Wizara ya Kazi na
Ajira kama Wizara inayohusika na ‘social security’. Hoja hii inatiliwa
nguvu na uhalisia kwamba Mdhibiti wa Mifuko
23
(SSRA) yupo chini ya Wizara ya Kazi. Vile vile Wizara ya Fedha kama
mlipaji mkuu wa Pensheni asiwe na Taasisi hata moja ya Pensheni chini
yake ili kuweka ‘checks’.
Mheshimiwa Spika, Hali kadhalika hakuna sababu ya kuwa na utitiri wa
mifuko mingi kama ilivyo sasa. Ipunguzwe na kubakia na mifuko miwili tu,
mmoja wa wafanyakazi walio katika sekta binafsi na sekta isiyo rasmi na
mwingine kwa wafanyakazi wa sekta ya umma. Tunarejea pendekezo letu
kwamba mifuko ya NSSF na PPF iunganishwe kuwa mfuko mmoja kwa ajili ya
sekta binafsi na sekta isiyo rasmi na mifuko ya PSPF, LAPF na GEPF
iunganishwe kuwa mfuko mmoja kwa ajili ya kushughulika na wafanyakazi wa
Sekta ya Umma”.
Mheshimiwa Spika, mojawapo ya vipaumbele vya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa
mwaka 2012/2013 ni kupunguza misamaha ya kodi ya kutozidi asilimia moja
ya GDP, kutokana na Mapato mengi ya Serikali kupotea kwa sababu ya
kutoa misamaha ya kodi kwa wadau mbalimbali wanaotakiwa kulipa kodi, na
ikizingatiwa moja ya michango ya waziri akiwa mbunge tarehe 25/8/2011
alisema “kupunguza misamaha ya kodi ya kutozidi asilimia moja ya GDP”.
Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini waziri alikuwa na nia ya dhati na
kukubaliana na Kambi Rasmi ya Upinzani uwezekano wa jambo hili. Hivyo
basi, ili kuonesha kuwepo kwa dhamira ya kweli Kambi Rasmi ya Upinzani
inataka waziri alijulishe bunge juu ya utekelezaji wa azimio hili.
6.0 MSAJILI WA HAZINA NA BODI ZA MASHIRIKA YA UMMA
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa mnamo mwaka 2010 Sheria namba 2 (the
written laws (miscellaneous amendments) No 2. ACT 2010 ilipitishwa na
katika eneo la kumi (part X) ilifanyia marekebisho sheria ya mashirika
ya umma (the public Corporations Act, CAP 257). Sheria hii ilisainiwa na
Rais mnamo tarehe 20 Mei 2010.
Mheshimiwa Spika, katika mabadiliko hayo ya sheria ibara ya 20 na 21
ilibainisha bayana majukumu ya msajili wa hazina na ndipo iliweka
majukumu yake ya kazi kuwa ni kusimamia mashirika yote ya umma. Aidha,
mabadiliko hayo yalibainisha wazi kuwa msajili wa hazina hatakuwa mjumbe
wa Bodi za mashirika haya na wala hapaswi kushiriki kwenye vikao vya
bodi vya mashirika haya kwani yeye ni msimamizi mkuu wa mashirika hayo
na anapaswa kusimamia utendaji kazi wake.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mabadiliko hayo ya sheria bado msajili wa
hazina amekuwa akihudhuria vikao mbalimbali vya bodi za Mashirika ya
Umma kama mjumbe jambo ambalo ni kinyume na sheria, na amekuwa
akishiriki moja kwa moja kwenye maamuzi ya bodi hizo jambo ambalo
linamfanya kushindwa kutimiza wajibu wake wa kuwa msimamizi kama ambavyo
sheria inaelekeza
25
Kambi ya Upinzani inataka kupata maelezo ya kina ni kwa nini hali hii
imeendelea kuachwa iwe ilivyo kwa msajili wa hazina kuendelea kuwa
mjumbe wa vikao vya Bodi za mashirika ya umma kinyume na sheria. Aidha
tunataka kauli ya serikali kuhusiana na suala hili.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapenda kupata maelezo ya Serikali kuhusu masuala yafuatayo.
Moja, Sakata la uuzwaji wa hisa za Shirika la UDA umefikia wapi?
Pili, Serikali imefikia wapi katika utungaji wa Sheria mpya ya Ofisi ya
Msajili wa Hazina ili kuimarisha usimamizi wa Mashirika ya Umma.
Tatu, Serikali imefikia wapi katika pendekezo la kuifanyia marekebisho
Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC) ili liweze kumiliki, kusimamia
na kuziendesha hisa za serikali katika Kampuni binafsi ambapo umiliki wa
Serikali ni chini ya asilimia 50. Pendekezo hili lilikuwa ni uamuzi wa
Bunge na hivi sasa mwaka mzima umepita bila Bunge kupatiwa taarifa
yeyote kinyume na maelekezo yake.
Nne, Serikali imefikia wapi katika utekelezaji wa Waraka namba moja wa
mwaka 2012 kuhusu usimamizi na uendeshaji wa Mashirika ya Umma na hasa
mahusiano kati ya Mashirika ya Umma na Wizara mama. Waziri wa Fedha kama
msimamizi mkuu wa Mashirika ya Umma amechukua hatua gani kuhakikisha
falsafa ya ‘eyes on, hands off’ katika kusimamia Mashirika ya Umma
inatekelezwa
26
kikamilifu na kuhakikisha Mashirika ya Umma yanaendeshwa kwa faida na bila kuingiliwa ingiliwa na Wanasiasa?
7.0 Ofisi ya Takwimu ya Taifa
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (National Bureau of
Statistics – NBS) ilizinduliwa rasmi tarehe 26 Machi, 1999 kama Wakala
wa Serikali (Executive Agency) kwa mujibu wa Sheria ya Wakala wa
Serikali Na. 30 ya mwaka 1997, (The Executive Agencies Act 1997) (Act
No. 30 of 1997), na ndio chombo rasmi kinachojihusisha na kutafuta,
kuandaa na kusambaza takwimu hapa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, katika kupanga mipango ya maendeleo na kuandaa sera
mbalimbali za nchi husika, upatikanaji wa takwimu rasmi zinazotokana na
Kanuni na Mbinu za Kitaalamu iliyowekwa na Ofisi ya Takwimu ya Umoja wa
Mataifa (United Nations Statistical Division) ni muhimu. Takwimu zote
zilizo rasmi duniani hutolewa na Ofisi za Takwimu za nchi husika kupitia
Sheria za Takwimu za nchi mbali mbali.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imekua ikitoa Mapendekezo ya
kuboresha utendaji wa Ofisi ya Takwimu katika Nyanja mbalimbali na
serikali kutothubutu kuchukua mapendekezo hayo na kuyafanyia kazi.
27
Mheshimiwa Spika, katika taarifa ya miaka hamsini ya wizara,taarifa
inaonesha wizara kuwa na nia ya kuboresha ofisi ya takwimu ya taifa kwa
kuboresha miundombinu ya utoaji takwimu nchini ,kuimarisha mfumo wa
takwimu nchini (NBS), kutoa takwimu sahihi na kwa wakati, kutokana na
nia hii ya serikali Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuzingatia
Ofisi ya Takwimu Kuwa na uhisiano wa moja kwa moja wa Ofisi ya Takwimu
ya Taifa na ngazi za Mikoa, Halmashauri za Wilaya, Kata na Vijiji
kurahisisha upatikanaji wa takwimu ili zisaidie katika kupanga mipango
ya maendeleo.
8.0 Mamlaka Ya Mapato-TRA
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba
Mamlaka ya Mapato Tanzania ijenge uwezo wa kukagua mahesabu ya kikodi
kwenye Kampuni za Utafutaji wa Mafuta na Gesi, Kampuni za Madini na
Kampuni za Simu ambazo uzoefu unaonyesha kuwa katika maeneo haya kuna
mbinu nyingi sana za kukwepa kodi.
Mheshimiwa Spika, kwa msisitizo mkubwa sana Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaitaka mamlaka ya Mapato Tanzania kushirikiana kwa karibu na
Mamlaka ya Mawasiliano nchini kukagua mapato ya Kampuni za simu na hasa
kampuni ambazo zinatoa huduma kwenye kampuni za Simu.
28
Mheshimiwa Spika, Katika mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Mawasiliano
kulikuwa na mjadala kuhusu namna ambavyo wasanii wa Tanzania
wanavyonyonywa mapato na Kampuni zinazotoa huduma ya miito kwenye
kampuni za simu. Bunge lako lilielezwa kwamba Biashara ya miito kwenye
simu ina thamani ya shilingi bilioni 43 kwa mwaka lakini msanii
anayetengeneza kazi zinazouzwa anapata asilimia 7 tu ya mapato hayo.
Mheshimiwa Spika, taarifa zaidi za ziada zinaonyesha kuwa kampuni ya On
Mobile yenye mkataba na Kampuni za Simu za Vodacom na Airtel kama
‘aggrigator’ wa miito ya simu yenye miziki ya wasanii hapa nchini
hailipi kodi kutokana na mapato yake. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali kutoa taarifa za kikodi za kampuni hii na washirika wake na
hatua ambazo Serikali imechukua dhidi yao. Kambi ya upinzani inashauri
pia kwamba Mapato yanayotokana na miradi kama hii kwenye Kampuni za simu
yawe ‘ring fenced’ na kutozwa kodi stahiki au kodi maalumu.
9.0 Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani-Internal Auditor General
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Mkuguzi Mkuu wa Ndani (Internal Auditor
General) iliyoanzishwa na mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2010
inakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikileta migongano
katika maeneo ya kiutendaji na uwajibikaji, sheria haipo wazi juu ya
upatikanaji wa mtaalam huyo kama
29
inavyotakiwa na sheria na 8 ya utumishi wa umma, kwa mfano kutangazwa kwa nafasi hizo na waombaji kufanyiwa usaili.
Mheshimiwa Spika, pamoja na utata wa uteuzi wa mkaguzi wa ndani kama
sheria ya utumishi wa umma inavyoelekeza mkaguzi wa ndani anasimamiwa na
Katibu Mkuu Hazina (Paymaster General) ambaye naye ni mkaguliwa- kwa
hiyo kunakuwa na mgongano wa kimaslahi uhuru wa ofisi ya mkaguzi wa
ndani inaweza kukosa uhuru Kambi Rasmi ya Upinzani inaishauri serikali
katika ofisi ya Mkaguzi wa Ndani (Internal Auditor General office)
ingepaswa iwe na bodi ambako maalumu wangekuwa wanaripoti ili kuweka
uhuru unaofaa.
Mheshimiwa Spika, wakaguzi wa ndani ni waajiriwa wa serikali na hufanya
kazi zao za ukaguzi kwa kipindi chote ambacho shughuli za serikali
zikifanyika, mfano; katika halmashauri wakaguzi hutakiwa kuwajibika
kuanzia upokeaji wa fedha kutoka hazina, hadi kutumika kwake, Kambi
Rasmi ya Upinzani inahoji serikali nini nafasi ya wakaguzi wa ndani kama
ubadhirifu wa fedha za umma umeendelea kuwepo kama ripoti za mkaguzi
mkuu wa hesabu za serikali zinavyothibisha?
Mheshimiwa Spika, katika ushughulikiaji wa matumizi mabovu ya rasilimali za umma serikali imekuwa legelege hasa pale taarifa
30
zinapotolewa na wakaguzi wa ndani ambao hutoa taarifa mara kwa mara na
seriakali kukaa kimya, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali
kutambua umuhimu wa taarifa hizi za wakaguzi wa ndani na kuhakiki
inachukua hatua stahiki pasipo kusubiri taarifa za mkaguzi mkuu wa
hesabu za serikali ambazo ukaguzi wake hufanyika kwa kuchelewa zaidi.
10.0 Utekelezaji wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012 Pamoja na Mpango wa Maendeleo kwa Mwaka 2012/2013
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya Wizara ya Fedha mwaka 2011/2012 fungu
Namba 50 wizara ilitenga shilingi bilioni 659 kwa ajili ya miradi ya
maendeleo na fedha zilizotumika hadi kufikia Juni 2012 ni shilingi
bilino 402.7 ambapo fedha za ndani zikiwa shilingi bilioni 78.65 sawa na
asilimia 11.9 ya bajeti ya maendeleo hivyo kutegemea fedha za nje
katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa asilimia 88.1. Kambi Rasmi ya
Upinzani, pamoja na Seriliali kutokubali kutumia mapato ya ndani zaidi
katika kugharimia miradi ya maendeleo, I azidi kushauri serikali kuwa na
Makati wa dhati wa muda mrefu wa kuachana na utaratibu wa kutegemea
misaada ya nje. Mkakati huo ulenge kuiongezea mapato kwa kutumia mbinu
mbalimbali za kodi.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya 2012/2013 serikali imetenga shilingi
bilioni 546.51 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo
31
ambayo ni pungufu kwa asilimia 18 ya bajeti ya mwaka 2011/2012 ambapo
serikali ilitenga shilingi bilioni 659. Katika bajeti ya 2012/2013 ni
asilimia 19.3 tu ya fedha za ndani ndizo zimeelekezwa kwenye miradi ya
maendeleo na asilimia 80.7 ya makadirio ni fedha za nje ikiwa ni mikopo
ya kibiashara na misaada. Kambi Rasmi ya Upinzani inahoji: ni maendeleo
yapi ambayo serikali inadhamiria kwa kutenga fedha ya maendeleo ambayo
ni pungufu kwa asilimia 18 ya bajeti ya mwaka jana?
Hitimisho
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inasisitiza umuhimu wa
kuisimamia vema Wizara ya Fedha katika kusimamia uchumi wa nchi. Tuna
imani kwamba Waziri wa Fedha ndugu William Mgimwa na Manaibu wake Mhe.
Janeth Mbene na Mhe. Saada Mkuya Salum wataweza kukabili changamoto
tulizoainisha katika hotuba yetu na kufanyia kazi mapendekezo ambayo
tumeyatoa. Tumeona dalili za Wizara hii na hasa Waziri na Manaibu wake
kusikiliza katika masuala ya Kikodi hivyo, tuna imani kwamba wataendelea
kusikiliza.
Kambi Rasmi ya Upinzani haitasita kutoa ushirikiano kwa lengo la kuleta
maendeleo katika nchi yetu. Hata hivyo, tutakosoa kwa nguvu zetu zote na
kuchukua hatua za kiuwajibikaji dhidi ya njama zozote za kudhoofisha
maendeleo ya Taifa na watu wake. Siku zote tutasimama upande wa wanyonge
na kuwasemea wasio na sauti,
32
Watanzania milioni 30 wanaoishi vijijini na kwenye dimbwi la Umasikini (The Bottom 30M).
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani naomba kuwasilisha.
……………………………………
Kabwe Zuberi Zitto (Mb)
Waziri Kivuli-Wizara ya Fedha
12.08.2012
KIAMBATANISHO A.
Sheria mbalimbali kuhusiana na fedha haramu
i. the establishment of the Permanent Commission of Inquiry, or Ombudsman, 1966;
ii. the Foreign Exchange Control Act 1966;
iv. the establishment of an anti-corruption squad in 1975;
v. the Economic Sabotage Act 1983;
vi. the Economic and Organised Crime Act 1984;
vii. the Proceeds of Crime Act 1991;
viii. the Leadership Code (Declaration of Assets) Act 1995;
ix. the appointment of the Presidential Commission of Inquiry into Corruption, 1996;
x. the BOT Circular to Banking and Non-banking Financial Institutions, No. 8 of 2000, on Money Laundering.
xi. the Drugs and Illicit Traffic of Drugs Act 1995;
xii. the Arms and Ammunition Act 1991;
xiii. the Mutual Assistance in Criminal Matters Act 1991; and
xiv. the Tanzania Intelligence and Security Act 1998.
xv. The anti-money laundering Act, 2007
xvi. the anti-money laundering (amendment) act, 2012